Translate

Tuesday, 7 August 2018

KUHUSU TOHARANI

Toharani ni mojawapo ya maeneo ambayo hayajaeleweka vyema kwa wengi wa wasio wakatoliki, na pengine hata wakatoliki wengine hawaelewi vizuri jambo hili. Lengo letu la kujifunza somo hili kwa kina sio kwa ajili ya majibizano, bali ni kuwa, Neno la Mungu linatuhimiza kuwa, kwa upole na unyenyekevu, pale watakapotufuata moja kwa moja kwa mashtaka haya na mengine kama haya, wale watakaohoji imani yetu katika Kristo, hatuna budi tuwe tumejiandaa  (tuwe tayari) kuitetea imani yetu kikamilifu kama wakristu wenye Kipaimara. Ni wajibu wa kila mkatoliki kuijua imani yake kwa usahihi ili uwe na amani wewe mwenyewe, na uwalete wengine kwenye imani sahihi kwa Kristo, sawasawa na 1 Petro 3:15.

WALE WANAOPINGA UWEPO WA TOHARANI WANADAI YAFUATAYO:
·       Yesu Kristu alimaliza kazi ya ukombozi wetu pale Kalvari hata alisema “imekwisha”,
·       Inakuwaje tunasema kuwa baada ya kufa mtu anaweza kusamehewa dhambi iwapo hakupokea msamaha huo wakati akiwa hai?
·       Mungu ambaye ni upendo, na mwenye huruma nyingi, na aliyekwisha kutusamehe dhambi zetu kwa njia ya maisha, mateso, kifo na ufufuko wa Mwanae Yesu, hawezi kuwatesa watu toharani kabla ya kuwafungulia milango ya mbinguni. Aya wanazotumia katika kutetea jambo hilo katika Biblia (Mungu wa huruma na msamaha) ni kama vile: 1 Yn 4:10, Yn 5:24, Yn 3:16, 1 Yn 1:9, Yn 5:24.
Hivyo je, wakatoliki wanaibeza huruma ya Mungu kwa kufundisha na kuamini kuwa kuna toharani?..... Tutaona jibu lake hivi punde.

Pingamizi lingine kuhusu fundisho hili ni kuwa inaonekana kama vile wakatoliki wanajihalalishia kwenda mbinguni hata kama wamekufa wakiwa na dhambi. Kutetea msimamo huu wapinga toharani hutumia aya za Biblia kama vile Lk 11:23, Yn 14:6 na Yn 3:18. Kwa watu hawa, baada ya kufa ni ama mbinguni ama motoni, hawaamini kama kuna njia ya katikati.
Pingamizi lingine linatokana na ile desturi ya baadhi ya wakristu kudhani kuwa kama kitu hakipo kwenye Biblia basi hawawezi na hatupaswi kukiamini (“sola scriptura”). Wanadai kuwa neno “toharani” halionekani kwenye Biblia ambayo ndiyo mwongozo wa imani yetu. Wanadai kuwa toharani ni mapokeo ya kibinadamu ambayo hao wakatoliki “wasiojua Biblia” walijitungia kwa faida ya viongozi wao wachache ili kupata fedha zinazotokana na kuomba Misa za wafu! (Ukweli fedha hizo sio nyingi za kutosha kutoa ushawishi wa aina hiyo, pili haziingii mfukoni kwa Padre moja kwa moja….)
Wanadai ni mapokeo ya kibinadamu kama yalivyo mafundisho mengine ya kikatoliki ambayo wanadai ni pamoja na:
-   Kusali kupitia watakatifu (hasa Mama Bikira Maria)
-   Rehema
-   Mamlaka ya Baba Mtakatifu ya kufunga na kufungua yanahojiwa yanatoka wapi.
-   Mamlaka ya Kanisa kufundisha (imani sahihi na mwenendo unaofaa hapa duniani)
-   Sadaka ya Misa Takatifu. Aya wanayopenda sana kuitumia katika kutushtaki ni Mt 15:6. Kitu cha muhimu hapa ni kuwa hawa ni wakristu wenzetu, sio wapagani. Wanaamini kuwa Yesu Kristu ni Bwana na Mwokozi wa maisha yao, na wanakuwa waangalifu sana kutunza “mapokeo” ya madhehebu yao ili wasiipoteze ile wanayoiamini kuwa ndiyo imani sahihi.
Haya mafundisho matatu hapo juu kwa pamoja yanahusiana kwa karibu sana na fundisho la marehemu wa toharani, ndiyo maana yanapingwa yote pamoja, maana huwezi kuamini mojawapo bila kujikuta umeshakubali na hayo mengine yaliyosalia. Kwa hiyo ili kurahishisha ubishi wa mtu yeyote anayetaka kuingia kwenye ubishi huu, suluhisho ni kuyakataa yote pamoja.







KWA HIYO TOHARANI NI NINI?
-   Je neno “toharani” liko kwenye Biblia?
-   Je, kuna mapokeo halali ama wakatoliki tunajitungia miongozo yoyote tunayotaka kwa faida ya viongozi wachache wa Kanisa, Aya hizo zinazotupa mamlaka hayo ziko wapi katika Biblia?
Toharani katika Biblia: Mt 18:32-34; Lk 12:59 (sawa na Mt 5:26); Mt 12:31-32, na hasa 1 Kor 3:11-15; pia Ebr 12:29, Ebr 12:12-23 (the spirit of the just made perfect).
Kwenye Agano la Kale (kwa lugha yake ya asili ya kigiriki) tunakutana na maneno mawili ambayo yanamaanisha mahali baada ya maisha haya lakini sio mbinguni; Neno la kwanza ni“Hades” = toharani (Kiebrania ni “Sheol”, na kilatini ni “purgatorium”= kiingereza “purgatory” na Kiswahili “toharani”. Neno la pili ni “Gehena” = Jehanam = ziwa la moto. Kwa hiyo jibu ni kwa neno “toharani” ndio limo kwenye Biblia uliyo nayo.
Je sadaka ya Yesu Msalabani inatosha kwa maondoleo ya dhambi? Jibu ni Ndiyo inatosha. Lakini ningependa kukuuliza swali pia, kwamba ndiyo ilitosha lakini kwa nini alimtuma Roho Mtakatifu baada ya hapo? Kututakasa. Kwa hiyo kumbe tunaweza kukubaliana kwa jambo muhimu hapa, kuwa baada ya ondoleo la dhambi tunahitaji kutakaswa. Ndiyo maana Bwana Yesu alimtuma Roho Mtakatifu baada ya kufufuka na kupaa mbinguni.
Katika vitabu 72 vya asili vya Biblia, kuna kitabu cha Makabayo, soma 2 Makabayo 12:42-43. Pia tunaendelea kuona kuwa kuna desturi ya wayahudi ambayo ipo hadi leo, ya kuwaombea marehemu wa toharani ili kuwasaidia katika utakaso wapokelewe mbinguni, sala wanayoiita “Kaddish”. Inasaliwa miezi 11 mfululizo tokea mtu anapofariki. DIni ya Kiyahudi ndiyo dini ya kweli kabla ya ukristo, wao walimjua Mungu wa kweli na kushika maagizo yake, manabii wote wa kale walikuwa katika utaratibu wa dini hiyo. Wakristo ni watoto wa Wayahudi kiimani, chimbuko letu ni Uyahudi. Agano la Kale linatokana na dini ya Kiyahudi. Tofauti yetu na dini ya Kiyahudi iliyoendelea baada ya kuja Kristo ni kuwa baadhi ya wayahudi walimkataa Kristo kwamba sio Masiha nab ado wanamsubiria. Wale waliompokea ndiyo wanaitwa “wakristo”, Sisi ndio waisraeli wa leo, taifa la kweli la Mungu na warithi wa haki yake.







Nadhani kuwa tatizo inaonekana siyo fundisho kuhusu uwepo wa toharani, bali tatizo ni kuwa Kanisa Katoliki linapigwa vita pamoja na mafundisho yake. Wengine wanafanya hivyo kwa kujua wazi wanachofanya na wengine hawajui kuwa wanapingana na Kristo mwenyewe wanayedai kumwamini.
Mafundisho ya wakristo waliotutangulia tangu wale wa kwanza kabisa wa karne ya kwanza na kuendelea hadi leo, yanashuhudia uwepo wa toharani. Kama wao walikosea, kweli na sisi tunakosea. Bali kama walikuwa sahihi, basi na sisi lazima tuko sahihi, kwa sababu Kanisa letu ni la Mitume na linatii na kufuata mtiririko wa Mapokeo Matakatifu kama inavyoelekeza Biblia (2 Wathesalonike 2:15). Kuna “Mapokeo” (“M” herufi kubwa) na “mapokeo” (“m” herufi ndogo), mapokeo M herufi kubwa hayawezi kubadilika (mfano Dogma au mafundisho ya Kanisa yasiyoweza kubadilika, bali mapokeo m hefuri ndogo huweza kubadilika (mfano mapadre kutokuoa, mavazi ya makuhani, mpangilio wa altareni wakati wa ibada, nk. Hizi ni desturi tu za Kanisa na zinaweza kubadilishwa kwa utaratibu maalum wa Kikanisa kwa maongozi ya Roho Mtakatifu ambaye ndiye mwalimu wa Kanisa). Kuna mapokeo ya kibinadamu na mapokeo ya ki-Mungu. Sisi wakristu hatupaswi kufuata mapokeo yoyote ya kibinadamu na hatupaswi kuyaacha mapokeo yak i-Mungu.

Mababa wa Kanisa wamefundisha na kuandika kuhusu toharani: Mitaguso Mikuu ya Kanisa imefundisha juu ya toharani (Lyons 1274, Florensi 1439-45 na Trento 1545-63).
Fundisho la toharani halipingani na fundisho lile lingine muhimu kuwa Mungu wetu ni wa upendo na huruma. “Ili kwenda mbinguni, ni lazima tujikane nafsi zetu, tuchukue msalaba, tumfuate Kristo” – je hayo sio mateso? Kama Yesu alimaliza yote haya mateso ni ya kazi gani kumbe? Ili kuwa mkarimu sio kujitesa? Kuna kujinyima katika kuwa mkarimu na kujinyima ni kujitesa kwa namna moja au nyingine. Haya, neno linguine maarufu linasema “Sadaka yenye nguvu ni ile inayouma”. Pia tukumbuke kuwa tunapotaka kukua kiroho, lazima kufanya mazoezi ya fadhila takatifu, ambayo ni majikatazo, kujinyima, kujitesa, kujiadabisha na kujidhili kwa namna mbalimbali ili kujitakasa mbele ya Mungu (Warumi 5:3-5)
Mbinguni hakuna uchoyo au dosari yoyote. “Kama Mungu angeturuhusu kuingia mbinguni na dosari, hilo lingetusababishia mateso makali sana”. Ni sehemu ya huruma ya Mungu kutupa toharani ili tujitakase vya kutosha kabla ya kuingia mbele ya uso wake, badala angetutupa motoni kwa dosari kidogo tu. Hivyo tunaenda toharani ili kujitakasa vya kutosha na kulipia uzembe wa matakaso tuliyoshindwa kuyafanya tukiwa duniani (Ufunuo 21:27). Toharani ni hatua ya mwisho wa utakaso kwa njia ya Yesu Kristo na kwa njia ya kifo chake msalabani. Divai mpya haiwekwi kwenye viriba vichakavu. Pia tuelewe vyema kuwa hata utakaso wa toharani ni matunda muhimu ya kazi ya ukombozi wa Yesu Kristo na kifo chake pale msalabani. Hakuna utakaso unaojitegemea usiomhusisha Yesu Kristo, iwe ni hapa duniani ama toharani. Kwa njia yake, pamoja naye, na ndani yake”ndipo tunapata kibali cha jambo lolota mbele za Mungu.
Kwa upande mwingine, kila kosa analotenda mwanadamu lina adhabu yake kwa namna mbili; adhabu ya muda na adhabu ya milele. Ile ya milele ndiyo iliyoondolewa kwa njia ya kumwamini Yesu Kristu, na baada ya ubatizo kwa njia ya maungamo (Sakramenti ya Kitubio). Adhabu ya muda inaondolewa kwa njia ya kujitakasa (matakaso mbalimbali). Unaweza kujitakasa na kumaliza deni lako lote hapahapa duniani ama ukaenda kulimalizia sehemu iliyobakia toharani. Deni la matakaso halimpeleki mtu jehanam bali toharani, ambayo kwa lugha nyepesi ni “sehemu ya matakaso”. Hataka makosa ya kidunia yana hukumu tofauti-tofauti mahakamani, kuna onyo, faini, kifungo ama kunyongwa, nk. Mungu ndie chanzo cha hekima yote ya kweli.
-   Ushirika wa watakatifu unatupatia nafasi ya kusaidiana kupunguza deni la matakaso kwa njia ya Mwili wa Fumbo wa Kristo.
Pia ni vizuri kupitia kwa ufupi HATUA ZA KUKUA KIROHO AU HATUA ZA MATAKASO AU NJIA YA KWENDA MBINGUNI, ambayo mwanadamu inabidi aipitie katika kumfikia Mungu. Hakuna njia nyingine ya kumfikia Mungu tofauti na njia ya Sala. Sala ni kuutafuta Uso wa Mungu. Katika sala ndipo chanzo chote cha makuzi na utakaso wa kiroho.







ULAZIMA WA KUJITAKASA KABLA YA KUMWONA MUNGU
Hatua za sala. Sala ya mdomo, sala ya tafakari/ tafakuri, sala ya moyo, sala ya ukimya /sala ya utulivu, sala ya kutwaliwa, sala ya kifumbo, nk. Hatua za kukua katika sala zinashabihiana na jinsi roho inavyokua katika utakatifu, yaani inavyozidi kumkaribia Mungu. Tangu kuumbwa kwako Mungu amekuandalia cheo ambacho ni stahiki yako mbinguni. Kila mtu ana cheo chake,“kwa baba yangu kuna makao mengi”. Kama ukifa bila dhambi ya mauti lakini bila kufikia cheo cha utakatifu ulichoandaliwa wakati wa kuumbwa kwako, unajigundua mwenyewe mara unapoingia katika ulimwengu wa roho (unapofariki dunia), na unaelewa mara kuwa unaupungufu wa kipimo gani na hivyo unachagua wmenyewe kwenda sehemu ya utakaso kabla ya kwenda mbele za Uso wa Mungu. Vivyo hivyo roho inayojiona kuwa na dhambi ya mauti, hutishika sana na kuukaribia Uso wa Mungu aliye Mtakatifu hivyo kwamba roho hiyo masikini inaona mara moja kuwa ni bora mara milioni kwenda jehanam kuliko kuukaribia Uso wa Mungu na hali yake chafu. Ndiyo maana inasemekana kuwa Mungu hamtupi mtu yeyote jehanam, maana yake ni kuwa mtu mwenyewe anachagua aende wapi maana unapoingia katika ulimwengu mambo yote yanakuwa bayana. Kuukaribia Utakatifu wa Mungu ukiwa na dhambi ni mateso makubwa sana kwa roho hiyo, ni heri zaidi kukimbilia mbali iwezekanavyo, mbali na Uso wake Mungu ambako ni Jehanam. Kwa roho hiyo hakuna sala inayoweza tena kuwasaidia wala kuwatakasa kwani ni roho “mfu”.
Maandishi ya karne za awali za Ukristo zinatuambia kuwa Mtk Monika alimwomba mwanae Augustino (Mtk, Askofu na Mwalimu wa Kanisa) aikumbuke roho yake mbele ya altare ya Bwana baada ya kifo chake, hilo ndilo jambo moja tu alilolitaka kwake baada ya kifo chake.
Yapo hata leo mahandaki ambamo wakristo wa kwanza walijificha, humo zinaonekana sala zilizoandikwa ukutani kwa ajili ya kuwaombea marehemu.
Ukisoma 1 Petro 3:19 utakuta habari za wababa wa imani waliokufa kabla ya kuja kwake Kristo. Katika Kanuni ya Imani tunakiri kuwa Yesu alishuka kuzimu. Eneo hilo sio jehanum ya milele, bali ni ile sehemu ya muda ya utakaso, alikwenda kuwaamsha ili waende nae mbinguni, baada ya kuwa ameshaifungua milango hiyo kwa kifo chake, wafufuke pamoja naye. “Amka wewe uliyelala……..”, “Kristo amefufuka, chimbuko lao waliolala”.
Tabia ya kupambanisha Kanisa Katoliki na Biblia sio nzuri hata kidogo, ni kukosa kuelewa mambo ya msingi kuhusu imani ya kikristu. Chimbuko letu sio Biblia, bali ni Mapokeo Matakatifu.
-   Mapokea Matakatifu ndiyo yaliyoizaa Biblia. Hivyo Biblia ni Mtoto wa Kanisa. Kanisa ndio nguzo na msingi wa ukweli. Biblia haisemi kuwa Biblia ndiyo nguzo na msingi wa ukweli, inasema nguzo na msingi ni Kanisa (rejea 1 Tim 3: 15).
-   Kanisa ni Mwili wa Fumbo wa Kristo.
-   Kanisa limetupatia Biblia yenye vitabu 72 na sio pungufu.  Hata hivyo Biblia hiyohiyo inatukumbusha kuwa sio kila kitu kimeandikwa humo (Yn 21:25)
-   Kanisa linachota mafundisho yake katika Biblia, Mapokeo Matakatifu (sio yote yaliyoandikwa katika Biblia) na Magisteria ya kanisa (ndio uongozi wa Baba Mtakatifu na jopo la maaskofu wanaomshauri).

KKK (KATEKISIMU YA KANISA KATOLIKI) INASEMA NINI KUHUSU TOHARANI?
Kifungu cha 1472-1473 (vifungu viwili, vinaeleza kuhusu matokeo ya dhambi ya muda nay a umilele, “double consequence of sin”)
Kifungu cha 1030-1032 (vifungu vitatu vinaeleza kuwa tunapunguza deni letu la matakaso kwa sala, matendo ya toba, matendo ya huruma, kuvumilia taabu na mahangaiko. Deni lolote linalobaki wakati wa kufa kwetu tunalimalizia tukiwa toharani)







MAMBO YA UFAHAMU KUHUSU ULIMWENGU WA ROHO:
-   Mateso ya utakaso hayafanani kati ya roho moja na nyingine, inategemea deni husika la utakaso lililobakia (vilevile jehanam mateso ya waliolaaniwa hayafanani, kwani huruma ya Mungu inafika hadi huko kwa namna ya ajabu, kuhakikisha kuwa kila mtu anapata haki yake, vinginevyo shetani angevuruga mambo)
-   Furaha ya watakatifu mbinguni ni kamili kwa kila mtakatifu lakini hailingani kati ya roho moja na nyingine. Huko nako kuna vyeo mbalimbali. Huo ni mpango wa Mungu na makusudi yake tokea milele.
-   Muda, nyakati, tarehe na miaka ni mambo ya ulimwengu huu. Ulimwengu ujao hakuna muda. “Kwa Mungu siku moja ni sawa na miaka elfu, na miaka elfu ni sawa na siku moja” (Mfano wa mtu aliyekaa toharani miaka 20, akamtokea rafiki yake aliyekuwa padre, baada ya masaa 6 kulalamika kuwa amemsahau kumwombea Misa). Mwingine aliyekuwa amekata tama ya kuishi kutokana na kuugua muda mrefu, aliomba sana kifo, Malaika akamtokea na kumwuliza achague kati ya kuteseka hapahapa duniani ili kumalizia deni lake la malipizi, au afe akalilipizie toharani kwa muda wa mwaka mmoja. Jamaa akachagua kufa na kulipizia toharani. Malaika alipokwenda kumfariji kule toharani, jamaa alimfokea “Malaika mwongo, uliniambia nitakaa humu mwaka mmoja, mbona ni miaka isiyopungua 20 tangu nije humu, namna gani nateseka mie”. Malaika akamjibu, Masikini wee, bado hata hawajauzika mwili wako!
-   Toharani ni hali ya muda ya kiroho. Ni hali, sio mahali.
-   Roho walioko toharani hawatamani kurudi duniani kamwe, japo furaha yao haifanani na ya mbinguni. Hawatamani kurudi kwa sababu duniani hakuna uhakika wa jambo lolote, wao angalau wana uhakika kuwa watakwenda mbinguni siku moja. Tena wanaona waziwazi hatari zilizoko duniani na wanafurahia tumaini lao la uhakika wa kumwona Mungu.
-   Hawana mashaka yoyote
-   Hawawezi tena kutenda dhambi yoyote
-   Hawana wivu
-   Hawawezi tena kujiombea. Lakini wanaweza na wanatuombea sisi ambao bado tuko duniani
-   Mara nyingine wanapewa ruhusa na Mungu ya kuwatembelea wanadamu duniani kwa sababu maalum. Mfano Maria Simma: (Yeye amekuwa akiwaona na kuwasiliana na marehemu wa toharani tangu ujana wake, sasa ni mzee. Mama huyu amewasaidia sana marehemu aliowafahamu na asiowafahamu wakati wa maisha yao hapa duniani, kwa kuwaombea Misa kwa idadi walizomtajia, sala, kutoa sadaka kwa niaba yao na majitoleo mbalimbali). Mifano hai mingine kama ya Maria Simma ipo.
-   Tolea matendo yako mema na sala zako kwa ajili ya kuwasaidia katika utakaso wako, nao watakurudishia mara dufu kwa ukarimu wako kwa kukuombea hapa duniani nap engine siku ambayo na wewe utajikuta uko huko toharani.
-   Mrehemu walioko toharani wana furaha sana kwa sababu wanajua kuwa hawawezi kutenda tena dhambi.
-   Hawana tena hamu ya kutenda dhambi (hamna vishawishi huko)
-   Wako karibu zaidi na Mungu kuliko sisi tulioko bado duniani (they can feel Him but they can not see Him yet)
-   Wanauona na wanaufurahia ukarimu wa Mungu
-   Wanatembelewa na Mama Bikira Maria mara kwa mara kuwatia moyo hasa siku za Jumamosi na Sikukuu zake
-   Malaika Mlinzi wa kila roho iliyoko toharani haiachi roho hiyo, huwa nayo kusubiria na kumtia mtu moyo hadi muda wa kuikabidhi roho hiyo kwa Mungu mbinguni
-   Furaha yao imechanganyika na mateso makali. Mateso yao yanatokana na ile hali ya roho kutamani kumkimbilia Mungu na wakati huohuo ile hali ya kujikatalia kumkimbilia Mungu hadi utakaso ukamilike. Roho wa toharani hawaiti mateso yao “mateso”, bali wako katika hali ya kuridhika.
-   Mang’amuzi haya tunayapata kutoka katika maandishi ya Mtk Katarina wa Genoa, yeye alionyeshwa toharani na aliwatembelea roho walioko huko mara nyingi na kuwahoji mambo mengi sana.
-   Mateso ya toharani ni makali sana kushinda mateso yote ya wanadamu wote duniani nay a wafiadini yakijumlishwa pamoja. Mateso mepesi kabisa ya toharani ni makali sana zaidi ya teso lolote ambalo mwanadamu anaweza kulipata hapa duniani
-   Roho walioko toharani huweza kufahamu kuwa ni nani wanaowaombea huku duniani
-   Dhambi kuu tatu zinazoiitia hasira ya Mungu na kupeleka roho nyingi toharani ni kutokuiheshimu Dominika kwa kufanya kazi (kutokupumzika), dhambi za uzinzi (mawazo, maneno, nk) na kufuru mbalimbali.
-   Kama toharani isingekuwepo kwa ajili ya kumalizia kazi ya utakaso, roho nyingi sana zingeenda jehanam. Toharani ni ushahidi mkubwa sana wa huruma ya Mungu kwetu.
-   Anayewasaidia roho walioko toharani anajipunguzia muda wake mwenyewe wa kukaa huko baadaye.







TUNAWEZAJE KUWASAIDIA ROHO ZA MAREHEMU WALIOKO TOHARANI?
-   Kutolea sala kwa ajili yao hasa kuwaombea Misa Takatifu, Njia ya Msalaba, Rozari Takatifu, nk
-   Kuwaambia wengine kuhusu mateso ya toharani na kuwaomba wawaombee
-   Kutoa misaada kama majitoleo kwa wasiojiweza kwa ajili yao
-   Kufanya matendo ya huruma kwa ajili yao (kama kutembelea wagonjwa, kuwasaidia wenye shida, kusali, kuvumilia taabu, nk)
-   Kuwakumbuka marehemu wetu mbele za Bwana nyakati muhimu za Ibada ya Misa Takatifu na kuwainua kwake kwa sala fupi za kimoyomoyo.,
-   Nk.
Watakatifu wengi wameonyeshwa toharani na jehanam, wengine wamewezeshwa kutembelea maeneo hayo na wameacha maandiko yao kuhusu waliyoyaona huko. Maono ya watakatifu yanalingana na mafundisho ya Kanisa Katoliki na yanasaidia kutoa uelewa zaidi kuhusu maisha baada ya hapa duniani, yanatutia moyo na kutuhimiza kuwaombea marehemu wetu kwa bidii. Pia yanatufundisha na kutuhimiza kuishi maisha matakatifu hapa duniani ili kufupisha muda wa kukaa toharani au kuepa toharani na kwenda mbinguni moja kwa moja.

Watakatifu (na wenye heri) walioonyeshwa toharani ni pamoja na
-   Mtk Faustina Kowalska, Mtk Margareta Maria Alakoki, Sista Maria Serafina, Katarina wa Genoa, Katarina wa Bologna, Mtk Lidwina, Mtk Lutgarda, Mtk Malaki, Anna wa Malaika, Mtk Getruda, Magdalena wa Pazi, Visent Ferra, nk.

TAKE HOME MESSAGE:
Orodhesha majina ya marehemu unaowafahamu, ndugu, jamaa na marafiki (wasiopungua 10) na uweke mikakati ya kuwaombea Misa Takatifu japo kila mmoja mara moja kwa mwaka au zaidi. Na pia uweke mkakati wa kuwaombea mara unapowakumbuka kila siku maishani mwako.
*****************************************




Share:

0 maoni:

Post a Comment

Copyright ©| MKATOLIKI KIGANJANI ||CONTACT US 0757195712 ||KILIMANJARO SKY TECHNOLOGIES| |JEMA SOFTWARE DEVELOPER |JEROME MASSAWE||EMMANUEL MALLYA