Rozari Takatifu - Sala zake na namna ya kuisali
UTANGULIZI
Ifuatayo ni mada fupi kuhusu namna ya kusali rozari takatifu ya Bikira Maria, pamoja na sala kuu zinazosaliwa wakati wa sala hii ya rozari. Wakati wa kusali unaweza kuongeza sala nyingine zifaazo kadri ya nafasi. Rozari takatifu husaliwa na wakristu kutafakari maisha ya Yesu na Maria yaani Fumbo la Ukombozi, hasa kipindi cha mwezi Mei na Oktoba. Inahimizwa kuisali kama familia kila siku. Tusali rozari tupate amani, wakosefu waongoke na wasiomjua Yesu Kristu wamjue na kuokoka.
MAELEZO YA JUMLA
Anza kusali Rozari kwa kuibusu miguu ya Bwana Yesu katika taswira (picha) yake Msalabani kisha fanya Ishara ya Msalaba (gusisha msalaba huo kwenye paji la so, kifuani, bega la kushoto na kwa kutumia msalaba wa rozari takatifu huku ukiwa unasema “Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina”.
Taja kwa ufupi nia za Rozari hii. Tangaza nia hizo kwa sauti kama mnasali wengi kwa pamoja, Mfano, “Tusali kuombea amani katika nchi yetu na ulimwenguni kote" au tutolee rozari hii kuwaombea wagonjwa wetu: au :tuwaombee wote walioomba tuwaombee" nk. Hiyo ni mifano tu. Au unaweza kutoa mambi kuendana na tendo lililotangazwa kwenye kumi husika la tendo la rozari, au namna nyingine itakayofaa.
Baada ya Sala ya Nasadiki pamoja na ya Baba Yetu, tunamwomba Mungu (Utatu Mtakatifu) fadhila za Imani, Matumaini na Mapendo, zikiambatana na Salamu Maria tatu. Mojawapo ya maneno yafuatayo hutumika:
“Mungu Baba utuongezee Imani. Salamu Maria, …… Mungu Mwana utuongezee matumaini, Salamu Maria, …… Mungu Roho Mtakatifu washa nyoyo zetu kwa mapendo yako, Salamu Maria, …..”
Au;
“Utuongezee Imani ee Bwana, Salamu Maria,…. Utuongezee matumaini ee Bwana, Salamu Maria,…. Uwashe nyoyo zetu kwa mapendo yako ee Bwana, Salamu Maria, …..”
Au;
“Salamu e uliyechaguliwa na Mungu Baba, Salamu Maria,….. Salamu e Mama wa Mungu Mwana, Salamu Maria,….. Salamu e Mchumba wa Mungu Roho Mtakatifu, Salamu Maria,……”
Nk.
SALA ZA ROZARI TAKATIFU
KANUNI YA IMANI
Nasadiki kwa Mungu, Baba Mwenyezi, mwumba mbingu na dunia. Na kwa Yesu Kristu, Mwanaye wa pekee, Bwana wetu; aliyetungwa kwa Roho Mtakatifu, akazaliwa na Bikira Maria, akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato, akasulubiwa, akafa, akazikwa, akashukia kuzimu; siku ya tatu akafufuka katika wafu; akapaa mbinguni; amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi; toka huko atakuja kuwahukumu wazima na wafu. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Kanisa takatifu katoliki, ushirika wa Watakatifu, maondoleo ya dhambi, ufufuko wa miili, uzima wa milele. Amina.
BABA YETU...
Baba Yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe; ufalme wako ufike, utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni. Utupe leo mkate wetu wa kila siku, utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea. Usitutie katika kishawishi, lakini utuopoe maovuni. Amina
SALAMU MARIA...
Salamu Maria, umejaa neema, Bwana yu nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote. Na Yesu Mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa na saa ya kufa kwetu. Amina.
ATUKUZWE BABA...
“Atukuzwe Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo na sasa na siku zote, na milele, Amina”;
EE YESU WANGU...
Ee Yesu wangu, utusamehe dhambi zetu, utuepushe na moto wa milele, ongoza roho zote mbinguni, hasa za wale wanaohitaji huruma yako zaidi”;
TUWASIFU...
“Tuwasifu milele, Yesu, Maria na Yosef”.
DAMU YA KRISTU..
Damu ya Kristu, iziopoe roho zinazoteseka toharani, izitie nuru ya uzima wa milele. Amina.
Au;
RAHA YA MILELE..
Raha ya milele uwape ee Bwana, na mwanga wa milele uwaangazie. Wapumzike kwa amani. Amina.
NB: Kama muda unatosha uimbwe wimbo wa Bikira Maria japo ubeti mmoja kabla ya kutangaza tendo linalofuata (kila baada ya makumi mamoja)
LITANIA YA BIKIRA MARIA
Bwana utuhurumie
Bwana utuhurumie
Kristo utuhurumie
Bwana utuhurumie
Bwana utuhurumie
Kristo utusikie
Kristo utusikilize
Mungu Baba wa Mbinguni, Utuhurumie
Mungu Mwana Mkombozi wa dunia Utuhurumie
Mungu Roho Mtakatifu Utuhurumie
Utatu Mtakatifu Mungu Mmoja Utuhurumie
Maria Mtakatifu utuombee
Mzazi Mtakatifu wa Mungu utuombee
Bikira Mtakatifu Mkuu wa mabikira utuombee
Mama wa Kristo utuombee
Mama wa neema ya Mungu utuombee
Mama Mtakatifu sana utuombee
Mama mwenye usafi wa moyo utuombee
Mama mwenye ubikira utuombee
Mama usiye na doa utuombee
Mama mpendelevu utuombee
Mama mstajabivu utuombee
Mama wa Muumba utuombee
Mama wa Mkombozi utuombee
Mama wa Kanisa utuombee
Bikira mwenye utaratibu utuombee
Bikira mwenye heshima utuombee
Bikira mwenye sifa utuombee
Bikira mwenye uwezo utuombee
Bikra mweye huruma utuombee
Bikra mwaminifu utuombee
Kioo cha haki utuombee
Kikao cha hekima utuombee
Sababu ya furaha yetu utuombee
Chombo cha neema utuombee
Chombo cha kuheshimiwa utuombee
Chombo bora cha ibada utuombee
Waridi lenye fumbo utuombee
Mnara wa Daudi utuombee
Mnara wa pembe utuombee
Nyumba ya dhahabu utuombee
Sanduku la Maagano utuombee
Mlango wa Mbingu utuombee
Nyota ya asubuhi utuombee
Afya ya wagonjwa utuombee
Kimbilio la wakosefu utuombee
Mtuliza wenye huzuni utuombee
Msaada wa waKristo utuombee
Malkia wa Malaika utuombee
Malkia wa Mababu utuombee
Malkia wa Manabii utuombee
Malkia wa Mitume utuombee
Malkia wa Mashahidi utuombee
Malkia wa Waungama dini utuombee
Malkia wa Mabikira utuombee
Malkia wa Watakatifu wote utuombee
Malkia uliyepalizwa Mbinguni utuombee
Malkia wa Rozari takatifu utuombee
Malkia wa amani utuombee
Mwanakodoo wa Mungu uondoaye dhambi za dunia,
Utusamehe ee Bwana.
Mwanakondoo wa Mungu uondoaye dhambi za dunia,
Utusikilize ee Bwana
Mwanakondoo wa Mungu uondoaye dhambi za dunia,
Utuhurumie.
Utuombee, Mzazi Mtakatifu wa Mungu,
Tujaliwe ahadi za Kristo.
Tuombe
Ee Bwana Mungu, utujalie sisi watumishi wako afya ya roho na mwili siku zote; na kwa maombezi matukufu ya Maria Mtakaatifu Bikira daima, tuopolewe na mashaka ya saa, tupate na furaha za milele. Kwa Kristo Bwana wetu, Amina.
SALAMU MALKIA...
Salamu Malkia, Mama mwenye huruma, uzima, tulizo na matumaini yetu, salamu. Tunakusihi hapa ugenini sisi wana wa Eva. Tunakulilia tukilalamika na kuhuzunika bondeni huku kwenye machozi. Haya basi, Mwombezi wetu, utuangalie kwa macho yako yenye huruma. Na mwisho wa ugeni huu, utuonyeshe Yesu, mzao mbarikiwa wa tumbo lako. Ee mpole, ee mwema, ee mpendelevu, Bikira Maria.
KUMBUKA...
Kumbuka, ee Bikira Maria mwenye rehema, tokea zamani zote haitambulikani kumeachwa mwenye aliyekimbilia ulinzi wako, mwenye aliyetaka msaada wako, mwenye aliyetaka maombezi yako. Nami nimetumaini kwako, nimekimbilia kwako, ee Mama yangu, Bikira asiye na mfano, nimekuja kwako, nasimama mbele yako mimi mwenye dhambi. Mama wa Neno wa Mungu, usiyachukie maneno yangu, uyapokelee, uyasikilize, ukanifanyizie. Amina.
SALA KWA MTAKATIFU YOSEFU (mwezi wa kumi isaliwe baada ya rozari)
Ee Mt. Yosefu mwenye heri, tunakimbilia kwako katika masumbuko yetu, na kisha omba shime ya Mchumba wako Mtakatifu, tunaomba pia kwa matumaini usimamizi wako. Kwa ajili ya mapendo uliyompenda Bikira Mtakatifu Mzazi wa Mungu, na kwa ajili ya kumtunza Mtoto Yesu, twakuomba sana, utuangalie kwa wema sie tuliokuwa fungu lake Yesu Kristu, tukakombolewa kwa damu yake. Tusimamie katika masumbuko yetu kwa enzi na shime yako.
Ee Mlinzi amini wa jamaa takatifu, uwakinge watoto wateule wa Yesu Kristu. Ee Baba uliyetupenda mno tuepushe na kilema chochote cha madanganyo na upotevu. Ee kinga yetu mwezaji, utusimamie huko juu mbinguni ulipo, tunaposhindana na wenye nguvu wakaao gizani. Kama vile siku za kale ukamwopoa Mtoto Yesu katika hatari ya kuuawa, na leo hivi likinge Kanisa Takatifu la Mungu katika mitego ya adui, na katika shida yote; mtunze daima kila mmoja wetu, tufwate mfano wako, ili tupate na msaada wako, kukaa na utakatifu maisha, kufa kifo chema, na kupata mbinguni makao ya raha milele. Amina.
TUNAUKIMBILIA...
Tunaukimbilia, ulinzi wako, Mzazi Mtakatifu wa Mungu. Usitunyime tukikuomba katika shida zetu, utuokoe siku zote kila tuingiapo hatarini, ee Bikira mtukufu na mwenye baraka. Amina.
0 maoni:
Post a Comment