Utukuzwe ee Bwana wangu Yesu Kristo./ Uliagua kifo chako./ Katika karamu ya mwisho ulitumia mkate wa kidunia/ ukafanya mwujiza na kuugeuza/ kuwa Mwili wako azizi./ Kwa mapendo ukawapa Mitume Mwili huo/ uwe kumbukumbu la mateso yako mastahivu./ Uliwaosha miguu kwa Mikono yako Mitakatifu./
Uheshimiwe, ee Bwana wangu Yesu Kristo./ Kwa kuhofu mateso na kifo,/ Mwili wako usio na kosa ulitoka jasho la damu/ badala ya maji./ Juu ya hayo uliutimiza wokovu wetu/ uliokuwa umetaka kuufanya./ Hivyo ulionyesha waziwazi mapendo yako/ uliyo nayo kwa wanadamu./
Utukuzwe, ee Bwana wangu Yesu Kristo./ Ulipelekwa kwa Kayafa,/ Wewe uliye Hakimu wa wote./ Ukaruhusu kwa unyenyekevu kutolewa kwa Pilato/ uhukumiwe naye./
Utukufu uwe nawe, Bwana wangu Yesu Kristo,/ kwa kuwa ulivumilia kuchekwa tena/ uliposimama huko,/ umevaa joho jekundu,/ umetiwa taji ya miiba mikali sana Kichwani,/ ukavumilia kwa saburi kubwa/ kutemewa mate katika Uso wako mzuri,/ kufumbwa Macho,/ na kupigwa mno na wajeuri/ ngumi na makofi Mashavuni na Shingoni./
Sifa iwe nawe, Bwana wangu Yesu Kristo,/ Kwa uvumilivu mkubwa ulikubali kufungwa nguzoni,/ kupigwa mijeledi kijeuri,/ kujaa damu na hivyo kusukumwa barazani kwa Pilato./ Ulionekana kama mwanakondoo asiye na kosa./
Heshima iwe nawe, Bwana wangu Yesu Kristo./ Umehukumiwa Mwili wako mzima/ Mtukufu wenye kutoka damu/ ufe msalabani./ Ulichukua msalaba kwa Mabega yako Matakatifu/ na kuumwa sana./ Kwa ghadhabu walikusukuma mbele/ mpaka mahali pa mateso,/ wakakunyang’anya nguo zako./ Hivyo ulikubali kupigiliwa msalabani./
Heshima ya milele upate Wewe,/ Bwana wangu Yesu Kristo./ Ulipokuwa katika taabu kubwa hii,/ ulimkazia Mama yako mstahivu/ Macho yako ya hisani na mapendo/ na unyenyekevu,/ ndiye Mama yako asiyekosa hata mara moja/ wala kukubali dhambi yeyote./ Ulimweka katika ulinzi mwaminifu/ wa Mfuasi wako ili kumtuliza./
Milele utukuzwe, ee Bwana wangu Yesu Kristo./ Ulipokuwa mwenyewe taabani,/ uliwapa wakosefu wote/ matumaini ya kuondolewa dhambi/ kwa kumwahidia mnyang’anyi aliyekuendea/ utukufu wa paradisi kwa huruma yako./
Sifa ya milele iwe nawe, Bwana wangu Yesu Kristo,/ kwa kila saa ulipovumilia uchungu/ na taabu kubwa mno msalabani kwa ajili yetu sisi wakosefu,/ maumivu makali sana/ yaliyotoka katika majeraha yako,/ yakapenya bila huruma Roho yako Takatifu./ Yakaingia kikatili katika Moyo wako Mtakatifu/ hata ukakatika,/ ukapumua Roho yako,/ ukainama Kichwa,/ ukaweka Roho yako mikononi mwa Mungu, Baba yako./ Na baada ya kufa uliacha nyuma Mwili baridi./
Utukuzwe, ee Bwana wangu Yesu Kristo,/ kwa Damu yako azizi na kwa kifo chako kitakatifu/ ulizifidia roho za watu,/ ukazitoa ugenini/ na kuzipeleka kwa hisani yako katika uzima wa milele./
Milele uheshimiwe, Wewe Bwana wangu Yesu Kristo./ Siku ya tatu ulifufuka katika wafu,/ ukajionyesha kwa wafuasi wako,/ ukapaa mbinguni/ mbele ya macho yao siku ya arobaini./
Shangilio na sifa ya milele upate Wewe, Bwana wangu Yesu Kristo,/ kwa kuwa umewapelekea wafuasi wako mioyoni mwao/ Roho Mtakatifu,/ ukawasha rohoni mwao mapendo makuu ya Mungu./
Pia, utukuzwe, usifiwe na kushangiliwa milele, Bwana wangu Yesu Kristo./ Umekaa katika ufalme wako wa mbinguni/ juu ya kiti cha enzi cha Umungu wako,/ ukaishi pamoja na Viungo vyako vyote Vitakatifu./ Na hivyo utakuja tena/ kuzihukumu roho za wazima na wafu wote./ Unaishi na kutawala/ pamoja na Baba na Roho Mtakatifu,/ milele. Amina.
0 maoni:
Post a Comment